Advertisement

Wanawake nchini Togo, wametakiwa kususia kitendo cha ndoa
kuanzia Jumatatu wiki hii kama njia ya kushinikiza serikali kuleta mageuzi.
Kampeini hiyo yenye kauli mbiu ”Juhudi za kuokoa Togo”
imeanzishwa kwa ushirikiano na mashirika tisa ya kijamii pamoja na vyama saba
vya upinzani pamoja na vyama vingine vya kijamii.
Kiongozi wa upinzani, Isabelle Ameganvi alisema kuwa kususia
ngono huenda ndio itakuwa silaha inayofaa kuweza kuleta mageuzi ya kisiasa.
Muungano wa vyama hivyo pamoja na mashirika yasiyo ya kijamii
unataka rais Faure Gnassingbe, ambaye familia yake imeshikilia madaraka kwa
miaka mingi waweze kuondoka mamlakani.

“tuna njia nyingi za kuwashinikiza wanaume kuelewa
tunachotaka sisi wanawake” alisema bi Ameganvi, kiongozi wa tawi la wanawake
la muungano huo.
Alisema kuwa yeye ameweza kushawishiwa na mgomo sawa na huo
nchini Liberia mwaka 2003,ambao walitumia njia ya kususia ngono kushinikiza
amani.
“ikiwa wanaume watakataa kusikia kilio chetu,
tutalazimika kufanya maandamano ambayo yatakuwa makali zaidi kuliko mbinu hii
ya kususia ngono.” aliongeza bi Ameganvi
Togo imekuwa ikiongozwa na familia moja kwa zaidi ya miaka
arobaini.
Rais President Faure Gnassingbe alichukua mamlaka mnamo
mwaka 2005 kufuatia kifo cha babake Gnassingbe Eyadema, aliyetawala Togo kwa
miaka 38. Rais alichaguliwa kwa muhula mwingine mnamo mwaka 2010.
Mgomo huo ulitangazwa katika mkutano wa hadhara mnamo siku
ya Jumamosi mjini Lome, na ambao ulihudhuriwa na maelfu ya watu.
Mkutano huo ulifanyika kupinga mabadiliko ya hivi karibuni
yaliyofanywa ambayo wakereketwa wanasema kuwa yatarahisisha ushindi wa chama
tawala cha Gnassingbe kuweza kwenye uchaguzi wa bunge utakaofanyika mwezi
Oktoba.
Wanaharakati wanasema kuwa mgomo huo utashinikiza wanaume
ambao hawajihusishi na mchakato wa kisiasa kuweza kuhakikisha malengo yake
yanatimizwa ambayo ni pamoja na kukomeshwa kwa utawala wa rais usio na kikomo.
Mapema mwezi huu, waandamanaji wanaopinga utawala wa rais
Gnassingbe walitawanywa na polisi kwa kutumia gesi ya kutoa machozi na wengine
zaidi ya miamoja wakakamatwa.
Source: BBC Swahili

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here