Advertisement

Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa amevunja ukimya na
kuzungumzia tuhuma mbalimbali zinazoelekezwa kwake, huku akisisitiza
kuwa sasa amechoka kukashifiwa. Alisema kuanzia sasa hatakubali
kuchafuliwa jina lake na mtu yeyote au chombo chochote cha habari na
atakayefanya hivyo, ajiandae kukabiliana na mkono wa sheria.

Lowassa alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa
habari nyumbani kwake katika Kijiji cha Ngarash Wilaya ya Monduli,
Arusha kuhusu tuhuma mbalimbali zinazoelekezwa kwake, ikiwamo ya kuandaa
na kuongoza mpango mkakati wa kumhujumu Rais Jakaya Kikwete.

“Imetosha. Sasa nimeamua kukabiliana na yeyote atakayenichafulia jina
na kunizulia mambo ya uongo. Nitatumia vyombo vya sheria na tayari
nimewaelekeza mawakili wangu kufanya hivyo,” alisema,

“Baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu sasa, nimeamua kuanza kuchukua
hatua mbalimbali za kisiasa na kisheria ambazo naamini zitatoa majibu
sahihi dhidi ya wale wote walio nyuma ya ajenda hizi chafu kwa lengo la
kuweka kumbukumbu sawia ndani ya chama changu na kwa jamii nzima ya
Watanzania ambao kwa muda mrefu wamelishwa mambo mengi ya kizushi na
wakati mwingine ya hatari dhidi yangu,” alisema.

Alisema tayari amepanga kuanza kuwasiliana na kuwasilisha malalamiko
yake kwa mamlaka husika zinazosimamia mienendo ya kimaadili na weledi wa
kitaaluma wa vyombo vya habari kama vile Msajili wa Magazeti na Baraza
la Habari Tanzania (MCT).

“Kama hiyo haitoshi, baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu nimeshaanza
kufikiria na kujipanga kuanza kuchukua hatua za kisheria dhidi ya
waandishi wa habari na wahariri ambao kwa makusudi wameamua kutumia
vibaya uhuru wa habari ambao serikali imeutoa. Naamini sote
tunakubaliana kuwa uhuru usio na nidhamu ni fujo.

Katika mkutano huo, Lowassa pia alikanusha madai kuwa hivi sasa yeye
na baadhi ya wanaCCM, wanakusanya taarifa na vielelezo vya mabaya ya
Rais Kikwete ili kuyawasilisha kwenye vikao vya chama.
Alisema katika mkakati huo, mahasimu hao wamekuwa wakivitumia baadhi
ya vyombo vya habari na kufikia hatua ya kudai kuwa ameanza kuandaa
orodha ya kile anachokiita madhambi ya Rais Kikwete ambayo wanadai kuwa
amepanga kuyasoma wakati wa kikao kijacho cha Halmashauri Kuu ya Taifa
ya CCM.

Alisisitiza kuwa ni jambo lisiloingia akilini kumhusisha yeye na kile
kinachoitwa mkakati wa kumhujumu Rais Kikwete au CCM ambacho alisema ni
mbunge anayetokana na chama hicho na kiongozi wa Kamati ya Bunge ya
Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.

“Kuhusu hili, napenda kusema kwa uwazi kwamba, mbali ya ukweli kuwa
sijapata kufikiria hata mara moja kuhusu hicho wanachokiita mabaya au
madhambi ya Rais, sina na wala siijui hiyo wanayoitaja kuwa ni orodha ya
mabaya ya namna yoyote dhidi ya Rais Kikwete,” alisema na kuongeza:
“Siyo kweli. Nampenda, namwamini na kumheshimu Kikwete ambaye urafiki
wetu haukuanzia barabarani kama baadhi wanavyodhani. Kwanza sijui
mabaya ya mheshimiwa Rais. Najua mazuri yake mengi lakini siyo mabaya,
hivyo sina nia ya kuyatafuta. Siwezi kumhujumu Rais wala chama changu.
Naamini hata mheshimiwa Kikwete pia hawezi kuamini uongo huo.”

Alisema awali, alikuwa akiyapuuza madai mengi yanayoelekezwa kwake
lakini amelazimika kuvunja ukimya kwani uongo ukizungumzwa mara nyingi
bila maelezo sahihi kutolewa, unaweza kugeuka kuwa ukweli na watu
wakauamini.

Richmond na kujivua gamba
Kuhusu tuhuma za kampuni ya kufua umeme ya Richmond na falsafa ya
kujivua gamba, Lowassa alisema atazizungumzia muda mwafaka ukifika
lakini, akasisitiza kuwa atafanya hivyo kupitia vikao rasmi vya chama.

“Mimi nimetumikia CCM kwa takriban maisha yangu yote tangu
nilipohitimu Chuo Kikuu Mlimani mwaka 1977. Ni kipindi cha zaidi ya
mwaka mmoja pekee ndicho nimekuwa nje ya mfumo wa chama nilipokuwa
Mkurugenzi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC). Najua kuwa
kupitia vikao ndiyo mtu unaweza kujenga hoja kukabiliana na zile
usizozikubali,” alisema.

Alisema hataki kuzungumzia masuala hayo nje ya vikao kukwepa kufanana
na baadhi ya viongozi wanaofanya hivyo kwa kutumwa na maslahi na utashi
binafsi kwa lengo la kujipatia umaarufu na kuchafua wengine.

Maandamano ya UVCCM Arusha
Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli alikana kuhusika kwa namna
yoyote na maandamano na malumbano yanayoendelea sasa ndani ya Umoja wa
Vijana wa CCM (UVCCM), unaomhusisha Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha, James
Ole Millya na makundi mengine akisema kipindi yanatokea alikuwa
Ujerumani kwa matibabu.

Hata hivyo, alishauri sauti za vijana zisipuuzwe kwani kufanya hivyo
ni hatari kwa chama na taifa kwa ujumla kutokana na uwezo wa kundi hilo
katika kufikiri, kuamua na kufanya mambo.

“Mzee Kingunge (Ngombale) alitufundisha kuwa vijana damu yao
inachemka haraka na uamuzi na matendo yao yanafanyika kwa mtindo huohuo
damu yao inavyochemka. Jambo muhimu ni kuwasikiliza, kujadiliana nao na
kuwarekebisha kwa amani pale wanapokosea, kamwe wasipuuzwe wala
kukaripiwa na kukandamiza mawazo yao,” alisema Lowassa.

Alitoa mfano wa maandamano waliyofanya enzi zao za ujana kupinga
ziara ya mmoja wa mawaziri wa Marekani aliyetembelea nchini akisema
licha ya kusukwasukwa na polisi, Mwalimu Julius Nyerere na Serikali yake
haikupuuza hata kidogo hisia, mawazo na kitendo chao.

Alisema iwapo kuna uvunjifu wa sheria uliotokea katika harakati za
vijana hao kuwasilisha mawazo na kutekeleza majukumu yao ni vyema sheria
ikachukua mkondo wake bila kuonekana wanatiwa kashkashi, kwani hakuna
aliye juu ya sheria.

Ugumu wa maisha na ukosefu wa ajira
Akirejea kauli yake aliyowahi kuitoa kuhusu ugumu wa maisha na
ukosefu wa ajira kwa vijana nchini, Lowassa alisema tatizo hilo ni bomu
linalosubiri muda wa kulipuka, iwapo hatua madhubuti na za haraka
hazitachukuliwa.

“Kama taifa tufanye uamuzi mgumu wa kukopa fedha kutoka taasisi za
ndani na nje, tujenge viwanda badala ya kusubiri uwekezaji kutoka nje
ambako nako kuna tatizo sawa na hili linalotukabili. Waasisi wetu
walifanya hivyo na kufanikiwa. Naamini sisi pia tunaweza tukiwa na nia
thabiti ya kukuza uchumi wetu na kuongeza ajira kwa vijana wanaohitimu
katika taaluma mbalimbali.”
Alisema hata Marekani na nchi za Ulaya zinazohimiza na kutekeleza
sera ya uchumi wa kibepari, zimeanza kuchukua hatua zinazofanana na
zinazotekelezwa katika ujamaa kwa kusaidia taasisi na kampuni za nchini
mwao ili kukuza uchumi wao na kulinda ajira za wananchi.


Kampeni za urais 2015
Akionyesha kushangazwa na kitendo cha mjadala wa mrithi wa Rais
Kikwete kutawala duru za siasa nchini sasa mwaka mmoja tu tangu
kufanyika uchaguzi mkuu, Lowassa alisema hiyo: “Si salama kwa nchi wala
amani yetu kila jambo nchini kutawaliwa na mjadala wa urais mwaka 2015.”

“Tumeacha kujadili mustakabali wa taifa kwa kutafuta ufumbuzi wa
matatizo yanayoikabili jamii yetu na hili ni changamoto kubwa kwa vyombo
vyetu vya habari ambavyo vinawajibu wa kuendeleza mijadala yenye tija
kwa taifa, badala ya kukubali kutumika na wanasiasa wenye malengo yao
binafsi.”

Alivitaka vyombo vya habari kuchukua jukumu la kuongoza mijadala ya
kusaidia jamii kutafuta ufumbuzi wa ajira kwa vijana, uchumi na kulinda
amani, utulivu na mshikamano alioeleza kuwa umeanza kutikiswa kwa
vitendo na maneno ya watu wachache wenye malengo binafsi dhidi ya
maslahi ya umma.

CHANZO: Mwananchi

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here